ASKARI WA JESHI LA WANANCHI, JWTZ WAFA NCHINI SUDANI.

9:40 PM
ASKARI watatu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wamekufa maji kwenye mji wa Darfur, Kusini mwa Sudan wakiwa katika Operesheni ya Kulinda amani katika nchi hiyo.  Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema kuwa, tukio hilo lilitokea juzi wakati askari hao pamoja na wengine wakiwa kwenye doria ya kawaida mchana ambayo ni sehemu ya majukumu yao ya kawaida wakiwa nchi humo.  Alisema katika doria hiyo, walitakiwa kuvuka Mto Malawasha ulioko katika Kijiji cha
Ahamada kuelekea maeneo jirani kabla ya kukutwa na ajali hiyo.

 Mgawe aliwataja waliokufa kuwa Sajini Taji Julius Chacha na Private Anthony Daniel ambao wote wanatoka Kikosi Jeshi 34 kilichopo Lugalo, Dar es Salaam. Mwingine aliyefariki ambaye hata hivyo maiti yake bado haijatikana, ni Koplo Yusuph Said kutoka Shule ya Mafunzo ya Infantilia, Arusha.

 “Ni kweli askari watatu, wamefariki Dunia, waliondoka wiki iliyopita kuelekea Jimbo la Darfur, Sudan kulinda amani, walikuwa kwenye operesheni ya kawaida ambayo inaratibiwa na Umoja wa Mataifa (UN), hivyo basi wakiwa nchini humo, askari hao wanakuwa chini ya Umoja huo,” alisema Mgawe.
Kwa mujibu wa mgawe, wakati tukio hilo linatokea, marehemu hao pamoja na wengine jumla yao wakiwa zaidi ya watano, walikuwa katika gari aina ya Deraya ambalo linafanya kazi ya doria, walipofika kwenye mto huo, walikuta kina cha maji kimepungua, jambo ambalo likawafanya waamini kuwa, maji yao ni kidogo na kwamba wanaweza kuvuka kama kawaida.

 Alisema, kutokana na hali hiyo, mmoja wao alishuka na kutembea ndani na maji hayo kwa ajili ya kupima kina, alivuka salama na kurudi kwenye gari hilo ili aweze kuwaruhusu wenzake kuvuka.  Alisema walipojaribu kuvuka tena kwa mara nyingine, ndipo maji hayo yalijaa ghalfa na kusababisha gari hilo kupinduka, jambo ambalo lilisababisha kila mmoja kutafuta njia ya kujiokoa.Chanzao; Mwananchi newspaper

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »